MKUU wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera, ameahidi kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), ili kutumia teknolojia zake za kisasa za mazao mbalimbali ili yaweze kuzalishwa katika mkoa huo.
Mazao hayo yale yanahitajika kutumika kama malighafi katika uchumi wa viwanda.
Homera alitoa ahadi hiyo wakati akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Tari, Dk. Geofrey Mkamilo, aliyemtembelea mkoani humo kuweka mikakati ya uzalishaji wa mazao ya chakula na ya kimkakati ikiwamo zao la michikichi, korosho, ufuta, alizeti na karanga kwa lengo la kusaidia uchumi wa viwanda.
Homera alisema wameshaanza mikakati ya uzalishaji wa mazao hayo katika wilaya zote ili kufanya mkoa huo kuwa na uhakika na usalama wa chakula pamoja na ziada.
Naye Dk. Mkamilo alisema wameshafanya utafiti wa mbegu za mazao mbalimbali ya teknolojia ya kisasa yakiwamo yanayohimili ukame na changamoto za wadudu, ambayo yameonyesha kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.
Alisema Tari imepewa jukumu la kuratibu zao la michikichi nchini ikiwamo kuzalisha mbegu zake na kuzigawa bure kwa wakulima.
Homera alimuahidi Mkurugenzi huyo wa Tari kuwa, wapo tayari kuwapatia eneo katika mkoa huo lenye ukubwa wowote kwa ajili kufanyika utafiti na ujenzi wa ofisi zake, na kuwataka kuwasilisha ombi hilo kwa kufuata taratibu.