Utoaji leseni za uuzaji gesi asilia kwenye vituo vya mitaani kwa kampuni binafsi uliokuwa uanze mwezi huu, umeahirishwa hadi mwezi ujao kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibii wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), mwanzoni mwa mwezi huu ilikuwa ianze kutoa leseni hizo, lakini umeathiriwa na mlipuko wa virusi hivyo, kwani waombaji walipaswa kutumia fomu za maombi kwa karatasi na sasa zitaanza kutolewa mwezi ujao kwa njia ya mtandao.
Hatua ya utoaji leseni imekuja baada ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutoa idhini kwa kampuni binafsi za mafuta, kufanya biashara ya kuuza gesi mitaani katika vituo vyao.
Vituo hivyo vinatarajiwa kuanza kutoa huduma ya kuuza gesi Juni, mwakani na tayari kampuni binafsi 24 zimeonesha nia ya kufanya biashara hiyo nchini.
Akizungumza na Habari- LEO Afrika Mashariki jana, Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo, alisema utoaji wa leseni kwa wafanyabiashara wanaotaka kuuza gesi asilia katika vituo vyao umechelewa kutokana na hali ilivyo na kwamba kwa sasa wanaendelea kuimarisha mfumo wa utaji leseni kwa njia ya mtandao.
Alisema mfumo huo unaofahamika kama ‘Licence and Order for System,’ unatarajiwa kukamilika katikati ya mwezi ujao na baadaye wataanza kutoa leseni baada ya maombi kutumwa mtandaoni.
Kaguo alisema kanuni na taratibu zitakazoongoza biashara hiyo zimeshakamilika, ambazo zinaendana na kuzingatia usalama kama ilivyo katika vituo vya mafuta ya petroli.
“Kwa sasa kanuni zipo tayari na leseni zitaanza kutolewa Mei katikati baada ya kukamilika uimarishaji wa mfumo wetu wa mtandao
na isingekuwa ugonjwa huu, watu wangekuwa wamepata leseni zao na kuanza kujenga miundombinu ya uuzaji,” alisema.
Awali, Meneja Biashara ya Gesi wa TPDC, Emmanuel Gilbert, alisema baada ya bodi ya shirika hilo kutoa idhini ya kufanyika biashara hiyo, kampuni zinazohitaji zinapaswa kupeleka maombi maalum ili zipatiwe idhini itakayoziwezesha kupata leseni Ewura.
“Gesi inatakiwa kuuzwa kwa bei isiyomnyonya mtumiaji, lakini na yeye (mfanyabiashara) apate faida, huku akihakikisha vituo hivyo vinakuwa na viwango kuepuka milipuko, hivyo lazima kubanwa na Ewura.”
“Baada ya kupatiwa leseni na Ewura, wafanyabiashara watapewa kipindi cha miezi sita ya uagizaji vifaa vya ujenzi na baadaye kuanza ujenzi, kwani vifaa hivyo unaagiza ndio unatengenezewa, hivyo Februari, mwakani ujenzi unatarajiwa kuanza,” alisema.