News News

Back

MARUFUKU KUNUNUA KARAFUU KWA WAKULIMA

26 May 2020
Habari Leo
Image

Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) limesema ni makosa kwa mujibu wa sheria ya Karafuu No.11 ya mwaka 2011 kwa mtu binafsi ikiwemo wafanyabiashara kununua karafuu kutoka kwa wakulima.

 

Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC, Dk Said Seif Mzee amesema hayo baada ya wafanyabiashara kununua karafuu kwa wakulima huku wengine wakipita vijijini na kujifanya ni wakala wa shirika hilo.

 

Amesema ZSTC ndiyo shirika lenye mamlaka kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2011 kununua karafuu kutoka kwa wakulima tangu mwaka 1968 ambapo shirika hilo lilianzishwa rasmi kwa mujibu wa sheria.

 

Alisema wanaofanya hivyo wajue wanakwenda kinyume na sheria na watakapobainika watachukuliwa hatua za kisheria na kuingia katika makosa ya wahujumu wa uchumi na kosa la kufanya magendo.

 

“Nawajulisha wananchi ZSTC ndiyo ina mamlaka na jukumu la kununua karafuu zote kutoka kwa wakulima kwa mujibu wa sheria Na.11 ya mwaka 2011 na halijateua wakala wa kazi hiyo,'' amesema.

 

Alisema, kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu atakayetiwa hatiani akijishughulisha na kununua mwenyewe zao la karafuu atalipa faini ya Sh milioni 10 au kwenda Chuo cha Mafunzo miaka isiyopungua mitano.

 

Alisema ZSTC inaendelea na kazi ya kununua karafuu kutoka kwa wakulima ambapo tayari tani 4,000 za karafuu zenye thamani ya Sh bilioni 62 zimenunuliwa katika msimu uliomalizika mwezi uliopita.

 

Alisema si kweli kwamba shirika limeshindwa kununua karafuu kutoka kwa wakulima na kwmaba ndiyo sababu baadhi ya watu wameamua kutumia kisingizio cha kununua karafuu hizo kwa njia ya ulanguzi. Alisema vipo vituo vya kununulia karafuu 33 vinafanya kazi wakulima wakivitumia kuuza karafuu zao.

 

''Hatujasitisha ununuzi wa karafuu kutoka kwa wakulima, vituo vyetu 33 vinafanya kazi Unguja na Pemba kununua karafuu za wakulima hivyo hawana sababu za kuuza karafuu hizo kwa walanguzi,'' alisema.

 

ZSTC inaendelea kununua karafuu kutoka kwa wakulima kilo moja kwa Sh 14,000 licha ya bei ya zao hilo kushuka katika soko la dunia.