Serikali imepiga marufuku kwa wafanyabiashara na kampuni kutoka nje ya nchi kununua mazao moja kwa moja kwa mkulima na badala yake wanunue mazao katika soko la upili.
Pia imetangaza kuvifutia usajili wa vyama vya ushirika 3,338 ambavyo ni hewa ikiwa ni baada ya kuisha notisi ya siku 90.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga jana alipokuwa akizungumzia kuhusu maendeleo ya vyama vya ushirika ambapo alisema kutokana na kuanza msimu wa mavuno, kuna taarifa ya wafanyabiashara na kampuni kutoka nje ya nchi kusambaa kwenye vijiji na kununua mazao moja kwa moja kutoka kwa mkulima na kwa bei ya chini.
Hasunga alisema wafanyabiashara wa ndani wenye leseni za kununua mazao ndio wanaopaswa kununua mazao kwenye soko la awali ambalo ni moja kwa moja kutoka kwa mkulima na kwa bei nzuri.
“Vijiji vinapaswa kutenga eneo ambalo wakulima watalitumia kuuza mazao yao kwa wafanyabaishara wa ndani wenye leseni kutoka halmashauri husika na hawa wanatakiwa kununua kwa bei nzuri.
“Wafanyabiashara wa ndani, ndio wanaopaswa kuuza mazao yao katika soko la upili, hatua ambayo wafanyabiashara na kampuni za nje ya nchi zinatakiwa kununua hapo, na hapo ndipo ambapo ushuru unatakiwa kutolewa kwa wafanyabiashara wa ndani na wanunuzi kutoka nje,” alisema Hasunga.
Aliongeza: “hivyo ni marufuku kwa kampuni na wafanya biashara kutoka nje kwenda kununua mazao ya debe moja au mbili kutoka kwa mkulima, kazi hiyo itafanywa na wafanyabiashara wa ndani na hii ndio njia ya kuwainua wafanyabiashara wetu.”
Aidha, alisema wafanyabiashara wanapaswa kununua mazao ya wakulima kwa bei ya kuridhisha na kuwa kinyume chake serikali itaingilia kati kutoa bei elekezi ili wakulime wasipunjwe.