News News

Back

SERIKALI YA KIRIA MFUMO WA KUUZA MAZAO NJE KIMTANDAO

14 May 2020
Nipashe
Image

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, amesema endapo ugonjwa wa virusi vya corona ukiendelea kwa muda mrefu, watalazimika kutumia njia ya mtandao kuuza mazao nje ya nchi.

 

Amesema pia watawatumia mabalozi wa Tanzania walioko nchi mbalimbali ambao watatafuta wafanyabiashara wakubwa na kuingia nao mikataba ya ununuzi wa mazao nchini.

 

Aliyasema hayo juzi bungeni wakati akijibu hoja za wabunge waliotaka kufahamu mikakati ya serikali katika kuyanusuru mazao ya biashara, ikiwamo korosho, pamba, chai, kahawa wakati huu wa ugonjwa wa virusi vya corona.

 

“Kama hali itaendelea hivi na wateja hawatafika nchini, tutatumia njia tatu za kuuza mazao yetu, mojawapo ni njia ya mtandao ambayo tutatangaza bei mtandaoni, wanunuzi nao watashindana, mwisho wa siku tutafika mwafaka na biashara itafanyika,” alisema Hasunga.

 

Kuhusu kuwatumia mabalozi, Waziri Hasunga alisema watawapa mamlaka mabalozi kutafuta wateja na kuingia nao mikataba ya manunuzi moja kwa moja.

 

Waziri Hasunga alisema matarajio ya wizara kwa mwaka ujao wa fedha ni kuhakikisha Tanzania inakuwa kinara wa uzalishaji wa chakula kwa nchi za Afrika Mashariki.

 

Alisema kwa mwaka wa fedha ujao wameweka malengo ya kuzalisha tani 400,000 za pamba, kutoka tani 352,000 zilizozalishwa mwaka huu.

 

Waziri Hasunga alisema kwenye zao la korosho wameweka malengo ya kuzalisha tani 350,000, chai tani 40,000, kahawa tani 90,000, miwa tani milioni 4.2.

 

Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM), Charles Mwijage, alisema mvua zinazoendelea kunyesha kwa sasa nchini zinatakiwa kuwa fursa katika kilimo cha umwagiliaji Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Fatma Toufiq, alisema miradi ya kilimo yenye changamoto inatakiwa kuundiwe tume ili iweze kuwa na tija kwa Taifa.

 

Naye, Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga, aliiomba Wizara ya Kilimo kutoa ufafanuzi kuhusiana na mfumo wa stakabadhi ghalani kwani umekuwa ukiwachanganya wakulima hususani wa zao la ufuta katika jimbo lake.

 

“Katika jimbo langu wananchi wa kata ya Mwaja na Yuga wanalima sana ufuta, walishazoe ufuta wao wanaenda kuuza, lakini serikali ikawakataza na kuwataka kuuza kwa mfumo wa stakabadhi ghalani hiyo inaleta taharuki sana,” alisema Mlinga na kuongeza:

 

“Mpaka najiuliza katibu wangu ana ajenda na nini katika jambo hili, wakati tunaelekea katika uchaguzi, natarajia kuwaeleza wanachi wangu ili tupate ufumbuzi wa jambo hili.”