News News

Back

TANZANIA, RWANDA KUSHUSHA MIZIGO MIPAKANI

19 May 2020
Habari leo
Image

Tanzania na Rwanda zimekubaliana kuwa mizigo yote inayokwenda Rwanda itashushwa katika vituo maalumu vya mipakani isipokuwa kwa mizigo inayoharibika haraka, bidhaa za mafuta na ile inayopitia nchini humo kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Hayo yameelezwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu makubaliano yaliyotokana na vikao vya pande hizo mbili vilivyokutana Mei 6 hadi 15.

Kamwelwe alisema makubaliano yaliyofikiwa yanataka mizigo inayokwenda Rwanda itashushwa katika vituo maalumu vya forodha vya mpakani; Rusumo na Kagitumba na kuhamishiwa kwenye magari mengine.

“Utaratibu huu hautahusu mizigo inayoharibika haraka pamoja na bidhaa za mafuta kama petroli, magari yanayobeba mizigo ya aina hiyo yataruhusiwa kuendelea na safari na yatasindikizwa bure hadi yafike kwenye mji husika ndani ya Rwanda,” alisema Kamwelwe.

Aliongeza: “Kwa magari yanayobeba mizigo inayopitia Rwanda kwenda DRC (transit cargo) yataruhusiwa kuendelea na safari na yatasindikizwa bure hadi mpaka wa Rwanda na DRC.”

Kamwelwe alifafanua zaidi kuwa: “kama mtakumbuka moja ya sharti lilitolewa na Rwanda ni kuwa mizigo hiyo isindikizwe kwa gharama ya dola za Marekani 500.”

“Sisi tuliwaambia tunakubaliana na hilo, lakini tukataka kiasi hicho kigawiwe kwa kilomita 160 ambazo ni za kutoka Rusumo hadi Kigali na kiasi kitakachopatikana kwa kilomita, kitumike pale magari ya mizigo ya Rwanda itakapokuwa nchini, ndio wakaondoa hoja hiyo na kuwa itasindikizwa bure,” alieleza.

Alisema makubaliano mengine ni kuwa magari ya mizigo yataruhusiwa kusafiri kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni hivyo magari hayataruhusiwa kutembea usiku.