News News

Back

TANZANIA, RWANDA KUUZA NYAMA ULAYA

13 May 2020
Habari Leo
Image

Tanzania na Rwanda kwa mara ya kwanza zitaanza kusafi risha nyama kutoka katika nchi hizo na kupeleka kuuza nchi za Ulaya kuanzia leo.

 

Usafirishaji wa nyama kutoka nchi hizo utafanywa kwa kutumia ndege ya mizigo ya RwandAir na utazinduliwa leo jijini Mwanza na Waziri wa Uchukuzi, Isack Kamwelwe, ikiwa ni mkakati wa kuingiza fedha za kigeni kutokana na mauzo hayo.

 

Akizungumza na HabariLEO Afrika Mashariki jana kuhusu masuala mbalimbali ya usafirishaji bidhaa katika nchi mbalimbali kutokana na changamoto ya ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, Kamwelwe alisema serikali inandelea na mazungumzo na nchi mbalimbali ikiwamo Rwanda, Uganda na Kenya, juu ya usafirishaji wa bidhaa katika nchi hizo.

 

Hata hivyo, alisema pamoja na changamoto ya virusi vya corona iliyopo, leo saa 10:30 alfajiri, ndege ya kwanza ya mizigo kutoka Rwanda itatua nchini kwa ajili ya kuanza usafirishaji wa nyama kwenda nchi za Ulaya kwa kushirikiana na nchi hiyo.

 

“Kiasi cha nyama kitakachoanza kusafirishwa, nchi zikakokwenda na utaratibu mzima wa ushirikiano na Rwanda nitaueleza kesho (leo) wakati wa uzinduzi, kwani jioni natarajia kuondoka kwenda Mwanza, huku Katibu Mkuu wangu akiwa tayari yuko huko kuendelea na maandalizi,” alisema.

 

Akizungumzia changamoto ya usafiri mipakani katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kamwelwe amesema bado kama jumuiya hawajajadili suala hlo, isipokuwa msimamo wa baadhi ya nchi unaendelea kuwa madereva wanaosafirisha mizigo wanapaswa kupimwa katika nchi husika na utaratibu huo hawajabadilika.

 

“Kila nchi ina utaratibu wake katika kuendelesha shughuli za usafirishaji, lakini jana (juzi) tulikuwa na mpango wa kufanya kikao cha mawaziri wa EAC kujadili suala hilo baada ya kutanguliwa na mkutano wa makatibu wa kuu wa nchi za EAC ili kupata suluhisho la majadiliano hayo,” amesema.

 

Kuhusu suala la Zambia kufunga mpaka kati yake na Tanzania, Kamwelwe amesema anasubiri taarifa rasmi kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini humo ili kulifanyiakazi suala hilo, kwani pia linahusu wizara ya mambo ya nje.