Wizara ya Viwanda na Biashara imeweka vipaumbele 10, kikiwemo cha kuendeleza na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kimkakati na vya kielelezo nchini.
Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2020/21 bungeni jana, Waziri Innocent Bashungwa alisema vipaumbele vingine ni kufufua viwanda vilivyobinafsishwa, kupanua na kukarabati vilivyopo na kuchochea au kuhamasisha uwekezaji au uanzishwaji wa viwanda vipya.
“Kuendeleza miundombinu ya msingi na saidizi ya maeneo ya uwekezaji na huduma ya viwanda kwa wawekezaji na wajasiriamali na uendelezaji na uwekezaji katika maeneo maalumu ya uwekezaji na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje,” alisema Bashungwa.
Pia kuendeleza taasisi za utafiti na maendeleo ya teknolojia ya viwanda na kuvutia na kuchochea matumizi ya teknolojia ya kisasa na kulinda viwanda na biashara za ndani dhidi ya ushindani usio haki.
“Kudhibiti ubora na viwango vya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini na zile zinazoagizwa kutoka nje na kujenga mifumo imara ya soko la ndani na kuhamashisha utafutaji na utumiaji wa fursa nafuu za masoko,” alisema.
Bashungwa alisema wizara imeweka mikakati 10, ukiwemo ya kuendeleza miundombinu ya maeneo ya uwekezaji nchini na kuendeleza utafiti na maendeleo ya teknolojia.
“Kuboresha mazingira ya biashara nchini, kulinda viwanda na biashara za ndani na kuimarisha ushindani, kushughulikia masuala ya ubora na viwango na kutafuta fursa za masoko na kuwaunganisha na wazalishaji wa ndani,” alisema.
Pia kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwapa elimu na mitaji, kuendeleza biashara na kuendelea kuwajengea uwezo watumishi.
Alisema sekta ya viwanda imeweka mikakati minane, ukiwemo wa kufanya tathmini ya utekelezaji wa Sera (SIDP) na mikakati ya mafuta ya kula, ngozi, nguo na mavazi na kutekeleza mkakati wa kuendeleza sekta ya viwanda.
Pia kusimamia na kufuatilia miradi ya kimkakati, kutekeleza mkakati wa kuvilinda viwanda vya ndani, kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika Maeneo Maalum ya EPZ/SEZ.
Alisema sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo imeweka mikakati tisa, ukiwemo wa kuendelea kufuatilia utekelezaji wa utengaji na uendelezaji wa maeneo kwa ajili ya uanzishaji wa viwanda vidogo na biashara ndogo kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
“Kuratibu uanzishwaji na uendelezwaji wa Kongano za Viwanda kwa ajili ya wajasiriamali, kukamilisha marejeo ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo na kuandaa mkakati wake,” alisema.
Pia kuimarisha au kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wajasiriamali, kuendelea kutafuta fursa za masoko ya ndani na nje kwa ajili ya bidhaa za wajasiriamali na kufanya utafiti juu ya mahitaji ya teknolojia kwa ajili ya uanzishwaji na uendelezwaji wa viwanda vidogo na vya kati.
Sekta ya biashara imeweka mikakati 13 ukiwemo wa kuendeleza majadiliano ya kibiashara kati ya nchi na nchi, kikanda na kimataifa kwa ajili ya kupanua fursa za masoko na uwekezaji ili kuvutia uwekezaji nchini.
Pia kuendeleza majadiliano ya biashara kwenye nchi za China, Urusi, Mauritius, Uturuki, Misri, Israel, DRC, Sudani Kusini, Vietnam na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kuingia nazo makubaliano ya biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi; pamoja na kuendelea na majadiliano ya kuanzishwa kwa Eneo Huru la Biashara kwa Nchi za Afrika (CFTA) na kukamilisha majadiliano ya kuanzisha Eneo Huru la Biashara la Utatu, linalojumuisha Kanda za COMESA, EAC na SADC.
Pia kukamilisha majadiliano ya biashara ya huduma kwa sekta sita za kipaumbele katika nchi wanachama wa SADC, kutekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja la EAC kwenye masuala ya biashara ya bidhaa na huduma; na kuratibu na kushiriki kwenye majadiliano ya biashara ya kimataifa katika mashirika yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa namengineyo ikiwemo WTO, UNCTAD, CFC na ITC.
Pia kuhamasisha Jumuiya ya wafanyabiashara kuhusu fursa za masoko ya upendeleo yatokonayo na majadiliano ya nchi na nchi, kikanda na kimataifa na kukamilisha utungaji wa sheria ya kujilinda kibiashara.
Pia kutekeleza Mkataba wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) unaohusu uwezeshaji wa Biashara, kukamilisha mapitio na kuanza utekelezaji wa Sera mpya ya Taifa ya Biashara.
Sekta ya Masoko imeweka mikakati saba ukiwemo wa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara, kuwaunganisha wazalishaji, wasindikaji na wafanyabiashara na masoko ya ndani na nje ya nchi na kupanua wigo wa matumizi ya mfumo wa stakabadhi za ghala.