News News

Back

VIWANDA 8,477 VYAJENGWA SERIKALI YA JPM

14 May 2020
Habari Leo
Image

Viwanda 8,477 vimeanzishwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Novemba 2015.

Kauli hiyo ilitolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara wakati ikijibu swali la Mbunge wa Mbulu Mjini, Zacharia Issaay (CCM).

Issaay alihoji je ni lini Serikali itaanza kufanya tathmini ya mafanikio ya viwanda 100 kwa kila wilaya ili kuchochea uchumi wa nchi yetu? Wizara hiyo ilisema serikali ilifanya tathmini ya jumla ya upimaji wa mafanikio ya azma ya ujenzi wa viwanda mwezi Februari, 2020.

Aidha, kati ya viwanda hivyo, viwanda vikubwa ni 201, viwanda vya kati ni 460 viwanda vidogo ni 3,406 na viwanda vidogo sana ni 4,410.

Ilisema Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, ilianzisha kampeni mahsusi yenye lengo la kufanikisha ujenzi wa viwanda vipya 100 kwa kila mkoa ; na si viwanda 100 kwa kila wilaya kama swali la msingi linavyouliza.

Vilevile, Wizara ya Viwanda kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, imeandaa mpango mahsusi wa kufanya tathmini pana ya viwanda vyote vilivyopo Tanzania Bara mwaka 2020/2021 kupitia utaratibu maalum, unaojulikana kama upimaji wa viwanda nchini.

Upimaji huo utafanya tathimini ya mpango wa viwanda 100 kila mkoa na utabainisha idadi na aina ya viwanda vilivyopo nchini.