News News

Back

WAKULIMA PARETO WAHAKIKISHIWA SOKO

14 May 2020
Nipashe
Image

Wakulima wa pareto nchini wametakiwa kuondoa hofu ya kukosa soko msimu ujao wa mavuno, kutokana na janga la virusi vya corona.

 

Badala yake wamehakikishiwa kuwa kuna biashara ya malighafi hiyo inazidi kuimarika duniani.

 

Hayo yalilezwa jana, jijini Mbeya na Mratibu wa zao hilo kutoka Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT), Michael Bishubo, wakati akizungumza na Nipashe kuhusiana na maandalizi ya kilimo cha zao hilo msimu huu.

 

Bishubo alisema licha ya uchumi wa dunia kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na janga la COVID-19, lakini soko la zao hilo halijatetereka kutokana na malighafi yake kuwa umuhimu pamoja na mahitaji makubwa duniani.

 

Alisema kwa sababu hiyo, wakulima hawatakiwi kuwa na hofu kuhusu uhakika wa soko kwa kuwa bidhaa ya zao hilo siku inatumika na watu ikiwamo kutengenezea sumu ya kuuliwa wadudu mashambani pamoja na majumbani.

 

Aliwataka wakulima kuhakikisha wanamaliza shughuli ya kupanda zao hilo kabla ya mwezi huu kumalizika ili kutoa muda wa kutosha kwa ajili ya kulihudumia zao hilo ikiwamo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

 

“Katika msimu huu kuanzia Januari ambao tulianza kupata mvua nyingi hadi Aprili ambao mvua zinaanza kupungua huwa ni msimu ambao tunawahimiza wakulima wetu kupanda pareto, kwa hiyo kwa muda huo hua wanaandaa miche kwenye vitalu,” alisema.

 

Kwa mujibu wa Mratibu huyo, Tanzania ina zaidi ya wakulima 16,000 wa pareto, huku idadi kubwa ya shughuli za kilimo cha zao hilo kikifanyika katika mikoa ya Songwe na Mbeya.