News News

Back

WAKULIMA WATAKIWA KUITUMIA VIZURI MVUA YA MASIKA

15 Apr 2020
Nipashe 15/o4/2020
Image

WAKULIMA wametakiwa kuitumia vizuri mvua ya masika inayoendelea kunyesha kwa kuotesha miche ya aina tofauti ya mazao ya kilimo licha ya kuwapo kwa janga la ugonjwa wa corona.

Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Dk. Makame Ali Ussi, alisema hayo wakati akifafanua mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu mvua ya masika inayoendelea kunyesha na wizara imejipanga vipi kutoa elimu kwa wakulima katika kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na ugonjwa huo.

Alisema njia pekee ya kukabiliana na ugonjwa huo ni kwa wakulima kuongeza bidii ya kuzalisha vyakula mbalimbali ili kukabiliana na tatizo la njaa.

Alisema hiki ni kipindi kizuri kwa wakulima kuongeza bidii na kuzalisha vyakula vingi ikiwa ni hatua ya kuchukua tahadhari na janga la njaa wakati taifa likikabiliwa na ugonjwa huo.

“Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi inawataka wakulima kuendelea kuzitumia vizuri mvua za masika kwa kuotesha miche ya aina mbalimbali na vyakula vya mazao ili kuliwezesha taifa kupata chakula kingi zaidi,” alisema.

Alizitaja juhudi zinazochukuliwa na Wizara ya Kilimo ni kusambaza kwa matrekta kwa ajili ya kusafisha mashamba ya mpunga kwa wakulima katika mabonde ya Unguja na Pemba.

Alisema hivi karibuni serikali imenunua matrekta 10 yenye uwezo wa kulima katika mazingira tofauti na hivyo kutoa fursa kubwa kwa wakulima kuendeleza kilimo cha mpunga.

“Matreka hayo tayari yapo mashambani kwa ajili ya kufanya kazi za wakulima, kusafisha

mashamba yao ikiwa ni sehemu za maandalizi ya kilimo cha mpunga,” alisema.