News News

Back

WAUZAJI GESI MAJUMBANI KUKATA LESENI

15 Apr 2020
Nipashe 14/04/2020
Image

Wauzaji wakubwa na wasambazaji wa gesi ya kupikia wametakiwa kukata leseni kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa ili kuhakikisha biashara hiyo inaendeshwa kwa misingi ya usalama na viwango vinavyokubalika.

Akizungumza na Nipashe, Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Hassan Juma Amour, alisema, kanuni hiyo imeweka vigezo maalumu kwa waingizaji na wasambazaji wa nishati hiyo ikiwamo kuwa na sehemu maalumu ya kuhifadhi mitungi ambayo itakuwa mbali na makazi ya watu.

Alisema vigezo ni lazima sehemu inapouzwa mitungi hiyo iwe na mitambo iliyokaguliwa na Wakala wa Mizani na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) ili kujua kuwa mitambo hiyo ipo salama kwa ajili ya kutia gesi katika mitungi.

Amour, alisema hiyo ni hatua ya pili ya kudhibiti sekta hiyo nchini ikiwamo hatua ya kwanza ya kuelimisha wadau jinsi ya kuendesha biashara hiyo kwa mujibu sheria na kanuni zao.

“Tayari tumeshakaa chini na waingizaji wakubwa, wasambazaji na wauzaji wa rejareja lengo ni kuwapa elimu na miongozo ya kuendesha biashara hii kwa misingi ya usalama na kuwafahamisha jinsi kanuni zinazovyoeleza usafirishaji na mambo mengine,” alisema.

Alisema zoezi hilo baadae litahusisha wauzaji wa rejareja ili kuona kila mtu anakuwa na leseni iliyokuwa kisheria.

“Tumeona kwanza tuanze kwa hawa waingizaji wakubwa kwa kuwa wauzaji wa rejareja wapo wengi na wao watakuwa mabalozi wazuri kwa hao wanaowasambazia,” alisema.

Alisema, hivi sasa soko la gesi ya kupikia hapa Zanzibar, limekuwa kwa kasi hivyo mamlaka imeona kunahitajika udhibiti na jambo hilo linahitaji kusimamiwa kwa nguvu zote kama inavyosimamia sekta ya mafuta.

Ofisa huyo alieleza kuwa, ZURA ina jukumu la kusimamia shughuli za nishati ikiwamo gesi ya kupikia majumbani ili kuona haileti madhara kwa watumiaji.