SERIKALI imezinganisha Benki ya TPB na TIB Corporate Ltd kuanzia jana, ikiwa ni hatua yake ya kuboresha utendaji wa mashirika na taasisi za Umma.
Hayo yalielezwa jana jijni Dodoma na Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka wakati wa kuelezea hatua iliyochukuliwa na serikali ya kuunganisha benki hizo.
Alisema serikali imechukua hatua hiyo kwa lengo la kuboresha utendaji wa benki inazozimiliki ili kuwa na benki moja ya biashara ambayo ni imara.
"Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utendaji wa mashirika na taasisi za umma ikiwamo kuunganisha taasisi zinazotekeleza majukumu yanayofanana ili kuongza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
"Kwa muktadha huu, kuanzia Juni 1 mwaa 2020, Serikali imeamua kuunganisha benki za TPB na TIB Corparate na kwa hatua ya awali benki ya TPB itachukuwa mali na madeni ya Benki ya TIB Corporate."
Mbuttuka aliongeza: "Muungano huu unalenga kuleta mageuzi makubwa ya kiutendaji, kimfumo, kimuundo, na kitaswira ili benki hii iweze kuhimili ushindani wa kibiashara kwenye sekta ya fedha."
"Wateja wote wa Benki ya TPB na Benki ya TIB Corporate wataendelea kuhudumiwa kwenye matawi yao ya sasa hadi hapo watakapotaarifiwa vinginevyo.
"Serikali inawahakikishia wateja wa benki hizi mbili pamoja na umma kuwa huduma za kibenki hazitaathirika kwa vyovyote vile kutokana na mabadiliko haya. Kuhusu wafanyakazi, Mbuttuka alisema hakuna mfanyakazi ambaye atapoteza kazi katika mabadiiko hayo.